MGOMBEA
pekee wa kiti cha uenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, amewaomba wanachama kumpa
tena ridhaa ya kuiongoza klabu hiyo ili iendelee kupata mafanikio chini yake.
Manji aliongeza kuwa, anataka kuendelea kubaki
Yanga ili kuiwekea mazingira ya kujitegemea na izidi kutisha katika soka ndani
na nje ya nchi.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika
kampeni zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kaunda yalipo Makao Makuu ya Yanga,
Manji alisema aliikuta timu hiyo ikiwa haina maendeleo lakini sasa inaogopwa.
“Tuliingia na ahadi ya kuzima utawala wa Simba,
wakati huo timu ilikuwa na migogoro, viongozi waliokuwepo walikuwa wakilumbana.
Ilikuwa Yanga mbovu, wengine wanajiuzulu.
“Lakini mimi na Sanga (makamu mwenyekiti
anayemaliza muda wake) kwa kuwa tulikuwa na mawazo sawa, tulipigana na matunda
yake ndiyo haya mnayoyaona,” alisema Manji.
Manji alisema endapo atachaguliwa tena,
atajitahidi kuweka mazingira ya Yanga kujitegemea ili iweze kufanya mambo yake
bila matatizo. Chini ya Manji, Yanga msimu huu imetwaa mataji matatu ambayo ni
Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA pia ipo hatua ya makundi ya Kombe
la Shirikisho Afrika.
Naye Sanga anayetetea kiti chake, akichuana na
Titus Osoro alisema: “Mambo tuliyofanya ni ushahidi tosha, nichagueni mimi na
Manji tuendeleze haya mafanikio tuliyopata.”
Katika uchaguzi huo utakaofanyika leo kwenye
Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar, jumla ya wagombea 20 wanawania nafasi ya ujumbe
wa kamati kuu ambapo wanahitajika nane tu.
Miongoni mwao ni, Lameck Nyambaya, Ayoub Nyenzi,
David Ruhago, Salum Mkemi, Samuel Lukumy, Tobias Lingalangala, Beda Tindwa,
Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ na Hussein Nyika.
Post a Comment