KWA
kiasi kikubwa Simba imeshamalizana na Kocha Mghana, Sellas Tetteh Teivi ili aje
kukinoa kikosi hicho msimu ujao katika safari ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu
Bara.
Sasa kali zaidi ni kwamba, kocha huyo ndiye
atakayetoa ruhusa ya kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Jackson Mayanja kwamba
aendelee na kazi au apigwe chini.
Teivi amewahi kukinoa kikosi cha timu ya
vijana ya Ghana na sasa akiwa na Sierra Leone amekabidhiwa hatma ya Mayanja
ambaye mkataba wake wa awali unamtambulisha kama kocha msaidizi.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema,
uongozi unasubiri ujio wa kocha mpya ili atoe pendekezo lake kama ataendelea na
Mayanja au atakuja na msaidizi wake kwani kila mwalimu ana falsafa zake.
Habari zinasema, sekretarieti ya Simba
imeliacha suala la Mayanja kwa Teivi ila wao sasa wanaendelea na mchakato wa
kumpata kocha mpya wa makipa.
“Suala la kocha msaidizi tumeliacha kwanza,
unajua makocha wengi wanapenda kuja na wasaidizi wao, iwapo huyu atakuja
mwenyewe, basi atafanya kazi na Mayanja lakini kama atakuja na mwenzake, haina
jinsi pia tunamsikiliza.
“Lakini sisi kama kamati (ya utendaji) kila
mmoja anataka Mayanja tuendelee naye kutokana na kazi kubwa aliyoifanya msimu
uliopita,” kilisema chanzo hicho.
Akiwa kaimu kocha mkuu akichukua mikoba ya
Muingereza Dylan Kerr, Mayanja aliiongoza Simba katika mechi 16 za ligi kuu na
kushinda 11, sare moja huku akifungwa michezo minne dhidi ya Yanga, Toto
African, Mwadui FC na JKT Ruvu.
Hakuna kiongozi wa Simba ambaye alikuwa tayari
kulitolea ufafanuzi suala hilo na hata ofisa habari wa timu hiyo, Hajji Manara
alipotafutwa alisema: “Nipo likizo hivyo sijui kinachoendelea klabuni.”
Post a Comment