KOCHA
wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amesema ana matumaini
na ameomba timu yake
isifanye makosa katika mchezo wa kesho
Jumapili dhidi ya MO Bejaia kwenye
Uwanja wa l’Unite Maghrebine jijini hapa.
Yanga inacheza na MO Bejaia mechi yake ya
kwanza ya Kundi A kuwania Kombe la Shirikisho Afrika na Pluijm raia wa Uholanzi
ana matumaini ya ushindi kwa kikosi chake.
Jambo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa
Yanga ni kuona beki wao mpya Hassan Kessy akiichezea timu hiyo kwa mara ya
kwanza akitokea Simba.
Katika mechi dhidi ya Yanga, Machi 20, mwaka
huu, Kessy akiichezea Simba alipiga pasi fupi iliyowahiwa na straika Donald
Ngoma (Yanga)
kisha akafunga na kuzua mjadala wa Kampa Kampa Ngoma.
Pluijm ana nafasi kubwa ya kumtumia Kessy
katika beki ya kulia ili kuziba nafasi ya Juma Abdul anayesumbuliwa na maumivu
ya enka, pia beki wa kati na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ hayupo kikosini
akitumikia adhabu ya kadi nyekundu.
“Baada ya kambi yetu ya Uturuki, tutaona
tulichopata, sitaki kumpa presha mchezaji yeyote yule. Soka ni mchezo wa
makosa, yeyote anaweza kufanya kosa na akajutia.
“Tunawajua wapinzani wetu na kuna sehemu
muhimu wapo makini na tayari tumezifanyia kazi, tuingie uwanjani na matumaini
ila hatutaki kufanya makosa,” alisema Pluijm, raia wa Uholanzi.
Katika mchezo wa kesho utakaochezeshwa na
mwamuzi Bouchaib El Ahrach raia wa Morocco, Pluijm anaweza kumtumia beki wa
kati Andrew Vincent ‘Dante’ katika nafasi ya Cannavaro akicheza sambamba na
Kelvin Yondani kwani Vincent Bossou anayetumika mara kadhaa, amefanya mazoezi
siku chache baada ya kuchelewa kujiunga na kambi ya Uturuki.
Yanga iliyoingia kambini Uturuki Jumapili
iliyopita, iliondoka nchini humo kuelekea Algeria ambako ilifika jana saa 7:00
mchana tayari kwa mechi ya kesho. Yanga inatarajiwa kupangwa hivi: Deo Munishi
‘Dida’, Kessy, Oscar Joshua, Dante, Yondani, Thabani Kamusoko, Simon Msuva,
Haruna Niyonzima, Ngoma, Amissi Tambwe na Deus Kaseke.
Katika mchezo mwingine wa Kundi A kesho, TP
Mazembe ya DR Congo itacheza na Medeama ya Ghana kwenye Uwanja wa TP Mazembe,
Lubumbashi, DR Congo.
Post a Comment