Wakati Yanga ikiendelea na harakati za kujiandaa na mchezo
wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, ghafla
kumeibuka mtafaruku baina ya nyota wa timu hiyo, Mrundi, Amissi Tambwe na
Mzimbabwe, Donald Ngoma.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinadai kuwa wachezaji hao
walivurugana na kufikia hatua ya kushikana na kudondoshana chini wakipambana
walipokuwa kwenye mazoezi ya timu hiyo huko nchini Uturuki walipokwenda kuweka
kambi.
Chanzo hicho kilikwenda mbali zaidi na kudai kuwa ingawa
sababu ya ugomvi wao haikujulikana tatizo nini lakini walionekana wakirushiana
maneno kabla ya baadaye kuvaana wakati programu ya mazoezi ya kocha Hans van
Der Pluijm raia wa Uholanzi ikiendelea.
Imeelezwa kuwa wakati ugomvi huo ukiendelea na Tambwe
akishikwa kwa ajili ya kutulizwa ndipo Ngoma alipopata upenyo na kumpiga Tambwe
usoni na kusababisha kumpasua katika paji lake la uso.
"Baada ya hapo ikawa tafrani lakini Tambwe ikabidi
atibiwe kwa ajili ya kumtuliza maumivu, baadaye kocha akazungumza nao kwa ajili
ya kuwatuliza na baada ya pale ishu ikapoa, lakini mpaka wanarudi Tambwe na
Ngoma hawakuwa kwenye mawasiliano mazuri," kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo, Ofisa Habari wa Yanga Jerry
Muro alipozungumza na Waandishi wa Habari, juzi Makao Makuu ya Yanga, Kariakoo
jijini Dar, alifafanua kuhusu ishu hiyo akieleza kuwa ulikuwa ni msuguano wa
kawaida ambao hutokea popote pale wachezaji wanapokuwa mazoezini.
"Hapana, haukuwa ugomvi, ilikuwa ni suala la
kuingiliana wakati wanafanya mazoezi, hutokea popote na hasa kwa timu yenye
ushindani kama Yanga maana Ngoma na Tambwe walikuwa wanacheza timu mbili
tofauti kwa hiyo kuingiliana vibaya kwa bahati mbaya wakati mnachuana ni
kawaida na hakukutokea ugomvi mkubwa.
"Tambwe na Ngoma wote wapo kikosi cha kwanza kwa hiyo
huwezi sema eti walikuwa na bifu kwa kugombania namba ndiyo maana wametibuana,
hapana, ni suala la mazoezini tu," alisema Muro.
Championi Jumatatu lilifanya jitihada za kuwatafuta
wachezaji hao kulitolea ufafanuzi suala hilo lakini Tambwe hakuwa hewani kwa
muda mrefu na hata alipopatikana hakupokea simu ya mkononi hata baada ya
kupigiwa zaidi ya mara mbili.
Ngoma naye alipotafutwa mara ya kwanza alionekana kuongea na
simu nyingine, alipopigiwa tena simu yake iliita bila ya kupokelewa.
Hata hivyo, Tambwe alipotua kwenye Uwanja wa Ndege akitokea
Uturuki usiku wa kuamkia jana alionekana akiwa na bandeji amefunga usoni, hali
ambayo inaonyesha ukweli wa suala hilo.
SOURCE: CHAMPIONI
Post a Comment