WAKIENDELEA
kuboresha kikosi chao, Simba wamepanga kuleta wachezaji sita wa kimataifa kwa
ajili ya kukiimarisha kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Kati ya wachezaji hao sita watakaoletwa na
Simba ni Janvier Besala Bokungu raia wa DR Congo, Blagnon Frederick kutoka
Ivory Coast na wengine wanne kutoka Afrika Magharibi ikiwemo Nigeria.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi
Jumamosi limezipata, nyota hao wanatarajiwa kutua wakati wowote kwa ajili
ya mazungumzo ya kusaini mikataba.
Chanzo hicho kilisema, nyota hao kabla ya
kusajiliwa wamepewa masharti ambayo ni kufanya majaribio kwa siku chache pindi
mazoezi ya timu hiyo yatakapoanza mwishoni mwa mwezi huu.
“Kila kitu kinakwenda vizuri katika usajili
wetu kwa maana ya kufanya usajili bab kubwa kwa kuzingatia mapendekezo
aliyotupa Kocha Mayanja (Jackson).
“Na usajili wetu tumepanga kuufanya kwa siri
kubwa kwa lengo la kuwahofia wapinzani wetu wengine kuja kutuharibia, maana
zipo baadhi ya timu zinazofanya usajili kwa kutuangalia sisi,” kilisema chanzo
chetu cha habari.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba,
Zakaria Hans Poppe hakupatikana hewani kuzungumzia suala hilo kwani kila
alipopigiwa simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa.
Post a Comment