Baada ya kuwatoa Shelisheli kwa
jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake mbili za kimataifa , timu ya soka ya
Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imebakiza mitihani
miwili kabla ya kuandika historia ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa
ya Afrika, imefahamika.
Mtihani wa kwanza ni mchezo
dhidi ya Afrika Kusini unaotarajiwa kufanyika ama Agosti 5, 6 au 7, 2016 ambako
mechi ya kwanza itapigwa ugenini kabla ya kurudiana jijini Dar es Salaam,
Tanzania wiki moja baada ya mchezo huo. Hivyo mchezo wa marudiano utafanyika
Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamzi Agosti 14, 2016 saa 9.00 alasiri.
Mshindi wa jumla katika michezo
hiyo, itacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville. Wakati
Afrika Kusini imepitishwa moja kwa moja Namibia imepenya kwa kuiondoa Botswana
licha ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wake uliofanyika jana Julai 2, 2016
huko Botswana.
Katika mchezo wa kwanza
uliofanyika Namibia, Juni 24, mwaka huu wenyeji (Namibia) walishinda 1-0. Kwa
msingi huo, Namibia imepenya kwa bao la ugenini ililolivuna katika mchezo wa
jana. Bao la ugenini imefanya kuwa na mabao 3-2.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys,
Bakari Nyundo Shime, ameangalia ratiba ya mlolongo huo na kusema “Ushindani
utakuwa mkubwa, lakini mimi nimelenga kushinda michezo yote iliyo mbele yangu.
Si kwamba napigania kufuzu kwenda Madagascar tu kwenye fainali za Afrika, la
hasha, nataka timu hii niipeleke Kombe la Dunia.”
Fainali za Kombe la Dunia,
mwakani zitapigwa India ambako kama Serengeti Boys itafuzu kucheza fainali za
Afrika na ikaingia nusu fainali kwa maana timu nne bora zote zitashiriki
fainali hizo ambazo tayari Tanzania imejiwekea mazingira mazuri ya kufuzu.
“Timu hii nimeanza nayo zaidi ya
mwaka mmoja. Sioni kama itakuwa kikwazo kuifanikisha kufika fainali za Kombe la
Dunia. Namuomba Mungu atunyooshee mkono wake, nawaombea viongozi wa TFF wazidi
kuihudumia timu hii, lakini pia wadau wengine waisapoti timu hii bila kuangalia
au kuchagua mtu anayeongoza TFF. Hii ni timu ya Watanzania wote,” amesema Shime
maarufu kama Mchawi Mweusi.
Shime alishukuru mipango na
ahadi ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
kugharamia kambi ya wiki mbili itakayofanyika Madagascar kuanzia Julai 24,
mwaka huu akisema: “Hii itakuwa ni kambi bora. Kwa sasa kikosi change
kinahitaji utulivu hivyo kwa maoni na mipango yangu naona inafaa.”
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya
Mpira wa Miguu kwa Vijana anayeongoza timu hiyo, Ayoub Nyenzi kadhalika aliomba
sapoti ya Watanzania ili kuendeleza timu hiyo, amesema: “Hakika nikipata watu
wakatusapoti, naamini ndoto zangu zitatimia .”
Nyenzi amethibitisha kwamba timu
hiyo itaondoka hapa jijini Victoria kesho Jumatatu Julai 4, 2016 saa 11.00
jioni Kisiwa cha Mahe miongoni mwa
visiwa 115 vya nchi hii ya Shelisheli na inatarajiwa kufika Tanzania saa 7.45
usiku wa kuamkia Jumanne Julai 5, mwaka huu.
“Wachezaji watakuwa na mapumziko
mafupi kabla ya kuanza kambi ya maandalizi kwenda Madagascar kwenye kambi ya
kuiandaa timu kucheza na Afrika Kusini,” amesema Nyenzi ambaye pia alijibu kuwa
watawapumisha nyota hao kwa ushauri wa makocha na daktari: “Mapumziko mafupi.
Msihofu”
Timu hiyo yenye wachezaji 20 na
viongozi wanane, itasafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia hadi
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Addis Ababa, Ethiopia kabla ya kubadili
ndege ya kuunganisha kwenda Dar es Salaam, Tanzania. Ikiwa Shelisheli ilifikia
hoteli ya Berjaya Beau Vallon Resort, iliyoko jijini Victoria. Hoteli ipo
umbali wa Kilometa 25 kutoka uwanja wa ndege.
Nyota waliosafiri ni pamoja na
makipa, Ramadhani Awm Kabwili na Samwel Edward Brazio wakati mabeki wako
Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick Mwenda, Dickson
Nickson Job, Ally Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba.
Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally Hamisi
Ng’anzi, Asadi Ali Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali,
Yassin Muhidini Mohamed, Shaban Zuberi Ada huku washambuliaji wakiwa ni Rashid
Mohammed Chambo, Mohammed Abdallah Rashid, Yohana Oscar Mkomola, Muhsin Malima
Makame Vitalis.
Hivi karibuni Serengeti Boys
ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa
yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya
kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika
Mashariki. Ilishika nafasi ya tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.
Post a Comment