Makapu kulia akipambana kwenye moja ya mechi za ligi kuu msimu uliopita

UNAWEZA kusema ni umafia baada ya uongozi wa Yanga kukubali kumpa mkataba wa miaka mitatu kiungo wake, Said Juma ‘Makapu’ baada ya pande zote mbili kufikia muafaka.

Kiungo huyo ambaye alitua Yanga misimu miwili iliyopita mkataba wake umemalizika hivi karibuni na kuna taarifa kuwa Simba nao walikuwa wakimtaka na walishafanya naye mazungumzo hali iliyowafanya Yanga waamke na kumpa mkataba haraka.

Chanzo cha karibu na uongozi wa timu hiyo kiiambia Tanzaniabettingarena kuwa, mabosi wa Yanga wameshakubali kumpa Makapu mkataba huo wa miaka mitatu, baada ya kuamini kuwa kutokana na umri wake atakuja kuwasaidia siku za baadaye.

Chanzo hicho kilisema haikuwa rahisi kupewa mkataba huo mrefu kwani katika mazungumzo yao kulikuwa na mvutano mkubwa, kuna baadhi ya viongozi walikuwa hawataki apewe mkataba huku wengine wakitaka apewe na ndipo wote wakakubaliana apewe.   

“Kila kitu kimeshakamilika na wanataka kumpa mkataba wa miaka mitatu kwani wanaamini kuwa kutokana na umri wake ataweza kucheza kwa kipindi kirefu lakini pia ni baada ya kusikia Simba nao wanamtaka na tayari walishafanya naye mazungumzo hivyo wakaona wasije wakawahiwa,” kilisema chanzo hicho.

Meneja wa mchezaji huyo, Yahaya  Tostao, alithibitisha kukamilika kwa dili la mchezaji wake ambapo alisema,: “Hilo la kumpa miaka mitatu ni kweli kabisa na sasa tumeshafunga mazungumzo na timu nyingine, kilichobaki ni kusaini mkataba tu lakini vitu vingine vyote vimeshafanyika, kati ya leo au kesho anaweza kusaini.”

Post a Comment

 
Top