WAKATI michuano ya Copa America ikianza leo, kikosi cha Brazil kimeendelea kupata majanga baada ya kiungo mshambuliaji Rafinha kuondolewa kikosini kutokana na majeraha.
Rafinha, anayechezea Barcelona ya Hispania, alidhaniwa angekuwa fiti kabla ya michuano hiyo kuanza akisumbuliwa na misuli ya nyuma ya goti la kulia.
Kiungo huyo aliumia baada ya kuangushwa na Radja Nainggolan wa AS Roma katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hivi karibuni.
Baada ya vipimo kadhaa, maofisa wa Barcelona wamethibitisha kwamba, Rafinha hatoweza kushiriki michuano hiyo maarufu barani Amerika.
Hili ni pigo kwa Brazil kwani ikiwa bila ya Neymar, itawakosa pia nyota kadhaa kama Kaka, Ricardo Oliveira, Ederson, Douglas Costa na sasa Rafinha.
"Nimejitahidi kuhakikisha nakuwa fiti kabla ya michuano hii, lakini kila kitu kimeshindikana hakuna jinsi, nitawafuatilia wenzangu nikiwa nyumbani,” alisema Rafinha.

Post a Comment

 
Top