Pasuwa |
KOCHA wa Simba, Mganda, Jackson
Mayanja amesema amekuwa akisikia kuwa Simba wanataka kumleta kocha Mzimbabwe na
anaamini kuwa anaweza kuisaidia timu hiyo.
Simba wamekuwa kwenye
mazungumzo na Kocha Kalisto Pasuwa ili aje awe kocha wao mkuu kwa ajili ya
msimu ujao huku Mayanja akisema hamfahamu lakini anaamini anaweza kufanya kazi
nzuri.
Simba imemaliza ligi ikiwa
nafasi ya tatu na sasa inataka kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao wa ligi ili
iweze kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
Mayanja aliyemaliza mkataba
wake klabuni hapo akiwa kama kocha msaidizi, baada ya kukabidhi ripoti kwa
kamati ya ufundi kwa sasa yupo kwao Uganda mapumzikoni, akisubiri hatma ya
mkataba wake mpya klabuni hapo.
“Simfahamu vizuri huyu Pasuwa,
lakini kama nilivyosikia kuwa Simba inafanya mazungumzo naye kwa ajili ya kuja
msimu ujao, hilo halina shida maana naamini atakuwa ni kocha mzuri tu na
anaweza kuisaidia timu.
“Kama nikiendelea kuwa Simba na
kuwa chini yake nitahakikisha timu inafika mbali, shida yangu ni kuona hizi
fedheha zinaisha, Simba nayo ipande ndege maneno yapungue,” alisema Mayanja.
Tayari imeripotiwa kuwa Simba
kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Pope, Wajumbe wa
Kamati ya Utendaji; Said Tully na Colins Frisch wapo nchini Zimbabwe kuzungumza
na baadhi ya wachezaji lakini pia kumalizana na kocha huyo mara baada ya
kumalizika kwa mchezo uliopigwa jana wa kufuzu michuano ya Mataifa Afrika
(Afcon), 2017 baina ya Zimbabwe na Malawi.
Post a Comment