SASA ni rasmi kwamba
Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro amefungiwa kwa mwaka mmoja kujihusisha na
mambo ya soka na kutakiwa kulipa faini ya Sh milioni tatu.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, jana
aliliambia Championi Jumamosi
kuwa, Muro amefungiwa na Kamati ya Maadili kutokana na kupingana na maelekezo
ya shirikisho hilo
Inaelezwa kuwa, Muro alipingana na maelekezo
ya TFF wakati wa maandalizi ya mchezo kati ya Yanga na TP Mazembe wa Kombe la
Shirikisho Afrika huku shitaka la kuishambulia TFF kwenye vyombo vya habari
likitupwa.
“Kamati imemfungia Muro kwa mwaka kujihusisha
na mambo ya soka na kutakiwa kulipa faini ya Sh milioni tatu lakini anayo
nafasi ya kukata rufaa kama hajaridhishwa na hukumu.
“Kisheria ndani ya wiki moja atapokea barua
yake na muda wowote kuanzia leo (jana) barua itamfikia mlengwa,” alisema Lucas.
Wakati hayo yakiendelea, Muro mwenyewe
ameliambia gazeti hili kwamba, hatambui hukumu hiyo kwani TFF wala kamati zake
hazina mamlaka ya kumsimamisha kazi.
Alisema bado anatambua kuwa yeye ni ofisa
habari wa Yanga miaka mingi ijayo na zaidi ya uongozi wa klabu hakuna wa kuweza
kumziba mdomo.
“Ngoja nifike mjini muone moto wangu, kwa sasa
niko kijijini narudi huko ili nionane nao. Siwezi kukata rufaa, kwanza ya nini
wakati hakuna kifungu cha katiba chenye mamlaka ya kunifungia mimi?” alihoji
Muro.
Post a Comment