Hans Poppe na Evans Aveva


UONGOZI wa Simba unaonyesha umepania kuimarisha nguvu ya kikosi chake kwa juhudi kubwa, sasa imepanga kumsajili beki wa kati wa timu ya taifa ya Malawi aliyetajwa kwa jina la Harry Nyirenda.
Nyirenda jana aliingoza Malawi ugenini kuivaa Zimbabwe na wenyeji wakashinda kwa mabao 3-0.
Zacharia Hans Poppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, pamoja na wajumbe Said Tully na Collins Frisch, jana walikuwa uwanjani wakati Zimbabwe ikiimaliza Malawi kwa mabao 3-0 na Nyirenda akionyesha soka safi.
“Ndiyo Nyirenda ni sehemu ya wachezaji ambao Simba inawataka na mazungumzo bado yanaendelea,” kilieleza chanzo.
Moja ya kazi kubwa kwa Hans Poppe na timu yake iliyosafiri kwenda Harare, Zimbabwe ilikuwa ni kufanya mazungumzo na beki huyo kwa ajili ya kuimarisha ukuta wa Simba.
Kamati ya usajili ya Simba pamoja na uongozi wa klabu hiyo, umekuwa ukihaha kuimarisha kikosi chao ambacho msimu uliopita kiliambulia nafasi ya tatu. Hali hiyo imeufanya uongozi wa Simba kuhakikisha unapata wachezaji bora huku ukipanga kuwatema wengi ambao walionekana ‘kuzingua’ mwishoni mwa msimu uliopita
Nyirenda sasa anaitumikia Black Leopards ya Afrika Kusini aliyojiunga nayo tangu 2010 akitokea MTL Wanderers ya kwao Malawi aliyoichezea kati ya mwaka 2009 hadi 2010.
Beki huyo ameanza kuitumikia Malawi tangu mwaka 2009 akiwa amecheza mechi tisa hadi sasa.

Post a Comment

 
Top