HATIMAYE kivumbi cha Ligi Kuu England kinatarajia kuanza leo ambapo timu kadhaa zitashuka dimbani ili kujaribu kuanza kuwania kutwaa taji la michuano hiyo.

Kwa sasa ubingwa huo unashikiliwa na Leicester City, ambao waliunyakua msimu uliopita baada ya kufikisha pointi 81, huku nafasi ya pili kienda kwa Arsenal, waliokamata nafasi hiyo baada ya kujikusanyia pointi 71.

Katika mechi za leo mabingwa watetezi, Leicester Ciy watakuwa ugenini  wakichuana na  Hull City katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa  KCOM, huku  Burnley wakichuana na  Swansea City, wakati Crystal Palace  wao watakuwa  na kibarua kizito mbele ya West Brom.

Everton watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani kuwakaribisha wakali wa Kaskazini mwa London, Tottenham Hotspurs, Middlesbrough  wao watakuwa kwenye Uwanja wao wa Riverside kuoneshana kazi na Stoke City, huku  Southampton nao wataburuzana na Watford. Man City wao watakuwa Etihad kuwakaribisha Sunderland.

Hata hivyo, pamoja na mechi hizo za ufunguzi, kuna upinzani wa aina yake, mtanange  utakaokuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa kandanda ulimwenguni kote ni ule utakaowakutanisha Arsenal dhidi ya watemi wa Merseyside, Liverpool.

Mchezo huo unatajwa kuwa utakuwa wa vuta nikuvute kutokana kuwa miamba hao wana wachezaji na makocha ambao wamejipanga ili kuhakikisha wanafanya vizuri msimu huu.

Mchezo mwingine utashuhudia Bournemouth wakiwaalika Man United ambayo kama zilivyo timu nyingine baada ya kufanya vibaya misimu kadhaa iliyopita, safari hii imejipanga  ili kuhakikisha inaondokana na msimu mbaya.

Post a Comment

 
Top