UKITAKA ubaya kwa mashabiki wa Simba kwa kipindi hiki, basi jipendekeze kuzungumzia mabaya juu ya mshambuliaji wao mwenye uwezo wa hali ya juu, Mrundi Laudit Mavugo.

Awali, mfalme wa Simba kwa kipindi cha nyuma alikuwa Mganda Emmanuel Okwi, ambapo tangu kuondoka kwake hakutokea fowadi mwingine aliyeweza kuzikonga nyoyo za mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi lakini sasa ameibuka Mavugo na kuonekana lulu.

Kabla ya mpachika mabao huyo kutua, jina lake lilivuma sana ambapo baada ya kufika nchini alidhihirisha ni kwanini viongozi wa Simba waliumiza vichwa mchana na usiku wakihakikisha wanainasa saini yake.

Mavugo amejizolea umaarufu mkubwa hivi sasa baada ya kuonesha cheche zake kwenye mchezo wake wa kwanza wa Simba Day dhidi ya AFC Leopards ya Kenya, uliomalizika kwa Simba kushinda mabao 4-0, huku Mrundi huyo akifunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao.


Kabla ya kutua ndani ya Simba, BINGWA lilikuwa mstari wa mbele katika kuripoti tetesi za Mavugo kutakiwa na Simba tangu msimu uliopita na sasa ametua rasmi, ambapo leo gazeti hili linakuletea mkanda mzima kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Ujio wa mavugo kwa mara kwanza

Taarifa za ujio wa mshambuliaji huyo zilianza kuvuma mwaka juzi, ambapo viongozi wa Simba akiwemo Makamu wa Rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Collin Frisch, walikwenda kufanya mazungumzo na Mavugo kwa ajili ya uhamisho.

Walipofika nchini Burundi, viongozi hao wawili waliingia makubaliano na Mavugo ya kusaini mkataba wa miaka miwili.

Lakini wakati viongozi wakiwa katika mazungumzo na mchezaji huyo, kumbe alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na mabingwa wa ligi ya Burundi, Vital’O na viongozi wa timu hiyo walihitaji dau kubwa ili kumwachia mchezaji huyo.

Kutokana na dau walilotaja Vital’O, Simba walishindwa na waliamua kumwacha ili amalize mkataba wake wa mwaka mmoja hadi hapo utakapomalizika na hatimaye wamalizane na mchezaji huyo ili aje nchini kujiunga na timu hiyo.

Zaidi ya kumwacha amalize mkataba wake huo, Simba tayari ilishamkabidhi Mavugo ‘kishika uchumba’ ambapo ilikuwa kiasi cha dola 2,000 za makubaliano yao.

Tetesi za kurejea tena

Mwaka mmoja uliopita na mwishoni mwa msimu uliopita kuliibuka tena tetesi za ujio wake ambapo mwandishi wa makala haya alikuwa na mawasiliano mazuri na mchezaji huyo.

Katika mawasiliano yao ya kila siku, Mavugo alimhakikishia mwandishi huyo kwamba atakuwepo katika kikosi cha Simba na kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara huku akiwaondoa wasiwasi mashabiki juu ya ujio wake.

Zaidi ya Mavugo kuondoa hofu hiyo, pia viongozi wa Simba nao walisimama kifua mbele kwa kuwatangazia mashabiki wa timu hiyo kuwa straika huyo atakuwepo msimu ujao.

Licha ya viongozi kuwaaminisha mashabiki kuwa Mavugo atatua Tanzania, bado haikuaminika kwa asilimia 100 na mashabiki walihitaji kumuona kwa mboni zao wakigoma kabisa kuamini ‘porojo’ kutoka kwa viongozi wao.

Wakati mashabiki wakikaa mkao wa kula kumsubiri Mavugo, BINGWA liliendelea kufanya mawasiliano ya kila siku na mchezaji huyo ambapo Mei 27, mwaka huu, Mavugo alikiri kuja nchini na kujiunga na Simba.

“Ni kweli mkataba wangu na Vital’O umemalizika na sasa nikimaliza mechi za Super Cup nitakuja Tanzania kucheza Simba,” hayo yalikuwa ni maneno ya Mavugo.

Baada ya mechi hiyo ya Super Cup kumalizika Mei 30 mwaka huu, ilizuka taarifa nyingine kwamba uongozi wa Vital’O umeliorodhesha jina la Mavugo katika orodha ya wachezaji waliokuwa nao msimu uliopita katika Shirikisho la Soka nchini humo.

Kuorodheshwa kwa jina la mchezaji huyo kuliwakosesha raha mashabiki wa Simba, pia rais wa Vital’O aliahidi kumpa Mavugo gari na nyumba ili aongeze mkataba mpya.

Aidha, taarifa nyingine ziliibuka kuwa Mavugo ameenda nje ya nchi kufanya majaribio, taarifa zilizozidi kuwanyong’onyesha Wanamsimbazi.

Safari ya Ufaransa

Kilichowafanya mashabiki wa Simba wasikitike kuhusu dili la Mavugo ni baada ya kusikia Mrundi huyo amekwenda Ufaransa huku viongozi wa Simba chini ya Rais Evance Aveva, wakiwa na ufahamu wa nini kinachoendelea juu ya mchezaji huyo.
 
Mavugo akiwa katika majaribio nchini humo, BINGWA liliendelea kuwasiliana naye akiwa nchini Ufaransa, ambapo Julai 20 mahojiano yenyewe yalikuwa hivi:

BINGWA: Hivi sasa umeenda Ufaransa, vipi kuhusu Simba?

Mavugo: Mpango wangu wa kuja Tanzania upo ila kwa sasa inategemea na majibu ya majaribio nitakayopata huku.

BINGWA: Majaribio yako yatakuwa ni ya muda gani?

Mavugo: Nimeambiwa ni ya siku saba, nitaendelea nayo na kama nitashindwa nitarejea nyumbani na kuja Tanzania kujiunga na Simba.

Agosti mosi mwaka huu, Mavugo alimthibitishia mwandishi wa makala haya kwamba ameshindwa masharti ya timu aliyokwenda kufanya majaribio na sasa amerejea jijini Bujumbura, Burundi na muda wowote atawasili Tanzania.

Sasa atua rasmi Tanzania

Usiku wa Jumatano, yapata saa 3 usiku, mwandishi wa makala haya alipata ujumbe kutoka kwa mchezaji huyo kupitia simu ya mkononi, ujumbe uliosomeka: “Nakuja leo Tanzania na nitatua na ndege ya saa 4:30 usiku.”

Baada ya mwandishi huyo kupokea ujumbe huo, alifunga safari hadi Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere na kushuhudia mashabiki wengi wa Simba katika eneo la tukio wakisubiri kumpokea mshambuliaji huyo, mikononi wakiwa na jezi yenye namba 45.

Simba Day

Hii ilikuwa ni siku maalumu kwa klabu ya Simba, hasa kwa mashabiki wa timu hiyo waliokuwa na hamu ya kuuona uwezo wa mchezaji wao huyo mpya kwa mboni za macho yao.

Licha ya kumuona uwanja wa ndege, bado mashabiki walikuwa na maswali mengi kwamba Mavugo aliyezungumzwa mwaka juzi ndio yule wa sasa?

Majibu ya maswali yao hayo yalipatikana baada ya kuingia katika kipindi cha pili cha mechi ya kirafiki dhidi ya AFC Leopards.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Mavugo alionyesha kiwango maridadi huku akifanikiwa kutoa pasi mbili na kuifungia bao moja katika ushindi huo mnono wa mabao 4-0.

Post a Comment

 
Top